WATOTO NA MIHADARATI

Sasa inabainika kuwa watoto walio na umri wa miaka 12 hapa Pwani wameanza kutumia dawa za kulevya.

Kituo cha kurekebisha tabia cha Reach out kinasema kimeanzisha kampeni ya kuwahamasisha watoto wa umri huo na kinalenga shule,huku hatua hiyo ikijiri kutokana na wazazi kutofahamu iwapo watoto wao  wameanza uraibu huo.

Murad Swaleh mwenye umri wa miaka 41 mwenyeji wa Mombasa hatimaye amefaulu kurekebishwa tabia baada ya kutumia dawa za kulevya kwa muda wa miaka 19.

Anakiri kuwa alianza na sigara, pombe na kisha heroine baada ya kukamilisha kidato chake cha nne na wazazi wake hawakugundua kuwa alikuwa na uraibu huo.

Mkurungenzi wa kituo hicho Taib Abdulraman asema inasikitisha kuwa wazazi hupuuza wanapofichuliwa na wasamaria wema kuhusiana na mienendo ya watoto wao na hata wengine kuwatetea dhidi ya uovu huo.

Sasa anasema wameamua kulenga wanafunzi wa umri wa miaka 12 na 15 walioanza kujitosa.

Haya yanajiri huku Swaleh akiwatahadharisha vijana wengine dhidi ya kutumbukia katika mtego huu na kusema kuwa haikuwa rahisi kujinasua kwa sababu alienda katika vituo vinne vya kurekebisha tabia kabla ya kurekebishwa pamoja na jamii kuwakubali.

Kulingana na twakimu zilizotolewa na mamlaka ya NACADA kuna watumizi laki moja wa hereoine katika eneo la Pwani huku ikikadiria kuwa wakenya laki saba wanatumia dawa za kulevya.

Total Views: 63 ,