WANAFUNZI ZAIDI WAJIUNGA NA SHULE ZA UPILI PWANI

Mpango wa serikali kuwataka wanafunzi wote waliomaliza darasa la nane mwaka jana kujiunga na kidato cha kwanza umefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika eneo la Pwani.

Kwa mujibu wa mratibu eneo la Pwani John Elunguta zaidi ya asilimia 82 ya wanafunzi kufikia sasa wamejiunga na shule za sekondari,tangu agizo hilo litolewe.

Mratibu huyo amesema kuwa utawala wa mkoa unaendelea kushirikiana na wakuu wa elimu wa kaunti ili kuhakikisha miundo msingi bora shuleni.

Hii ni baada ya wazazi kulalamikia uhaba wa madarsa ambayo hayawezi kukidhi idadi ya wanafunzi wanaozidi kuongezeka.

Kulingana na takwimu za sasa kaunti za Kwale na Kilifi zimejizatiti pakubwa katika utekelezaji wa agizo hilo.

‘’Kilifi imejaribu sana ,awali idadi ya wanafunzi hao ilikuwa ni asilimia 43 lakini sasa imeongezeka hadi asilimia 91 na kwale ilikuwa na asilimia 53 lakini sasa imefikisha asilimia 85 hapo’’.

Elunguta anasema yeye na maafisa wake watazuru kaunti ya Kwale siku ya Jumanne ili kuwapongeza maafisa nyanjani na kuwahimiza wanafunzi zaidi wajiunge na shule za sekondari.

Total Views: 66 ,