Siasa Kenya, Rais Uhuru na Raila Odinga kushirikiana

Ishara za ubora wa siasa za humu nchini zimejiri baada ya rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa Upinzani Raila Odinga kufanya mazungumzo ambapo cha msingi waliahidi kuliunganisha taifa kufuatia mgawanyiko uliojiri kutokana na uchaguzi mkuu.

Wawili hao wamesema kuwa ni wakati sasa kwa viongozi na wananchi kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuiwezesha Kenya kusonga mbele kimaendeleo kwa manufaa ya kila mmoja.

Wawili hao aidha wamesisitiza kuwa hawataruhusu misimamo na tofauti zao kuliangamiza taifa hili na kwamba ni wakati mwafaka wa kushinikiza mwanzo mpya kwa lengo la kuhakikisha kuwa ndoto za waanzilishi wa taifa hili zinaafikiwa.

Rais Uhuru na Raila Odinga walifanya mkutano wa faragha katika jumba la Harambee jijini Nairobi kabla ya kulihutubia taifa moja kwa moja kwenye kikao cha pamoja ambapo wamesisitiza kushirikiana baina yao kwa manufaa ya wananchi.

Hata hivyo mkutano huo uliwaacha wengi vinywa wazi huku Miguna Miguna akimuita Raila kuwa msaliti ilhali vinara wenza wakiahidi kupeana taarifa baadaye kuhusiana na mkutano huo wanaodai kuwashangaza.

Mwisho

Total Views: 283 ,