SHEHE AUNGA MKONO KITITA KWA WABUNGE WASTAAFU

Aliyekuwa mbunge wa Ganze Peter Shehe ameunga mkono mpango wa bunge la kitaifa wa kuwapa waliokuwa wabunge wa bunge la 11 jumla ya shilingi milioni 7 kila mmoja kama fedha za kuustafu.

Shehe anasema hela hizo zitawasaidia pakubwa wanasiasa hao,hasa baada ya kujitolea kuwahudumia wapiga kura wakati walipokuwa mamlakani.

Aidha ameongezea kuwa hela hizo ni haki kwa wabunge hao kwani walikuwa wakikatwa ushuru na ada nyinginezo wakati walipokuwa wakihudumu.

Mbunge huyo wa zamani amewataka wale wanaolalamika kuwa huenda mpango huo ukazidi kumgharimu mtozwa ushuru,kutokuwa na shaka kwani hela watakazopewa wanasiasa hao ni kama akiba yao waliyokuwa wakijiwekea.

Ameongezea kuwa ni haki kwa wanasiasa hao kulipwa fedha hizo kwani walikuwa watumishi wa umma kama wahudumu wengine serikalini.

Bunge,kupitia tume ya huduma za bunge (PSC),tayari limeiandikia wizara ya fedha itenge shilingi bilioni 2.1,kugharamia mpango huo utakaowafaidi wanasiasa wapatao 300.

Bunge linanuia kuipitisha azma hiyo punde tu litakaporejelea vikao vyake mnamo tarehe 12 Februari.

Awali mpango wa kuwalipa wanasiasa hao fedha hizo ulikuwa umesimamishwa na tume ya kutathmini mishahara SRC.

 

Total Views: 71 ,