Rais Uhuru Kenyatta ahifadhi Wadhfa wake

Rais Uhuru Kenyatta amehifadhi wadhfa wake baada ya kujizolea jumla ya kura 7,483,895 kwenye marudio ya uchaguzi wa urais wa tarehe 28 Oktoba.

Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Wafula Chebukati amesema kuwa idadi hiyo inadhihirisha asilimia 98.26 ya kura zote zilizopigwa kwenye shughuli hiyo na takriban asilimia 38 ya idadi ya wapiga kura waliosajiliwa.

Akizungumza baada ya kupokea rasmi cheti chake kama rais mteule, Uhuru amewapongeza wote waliojitokeza na kumpigia kura kwa mara ya pili akisema kuwa ni dhihirisho la imani yao katika utendakazi wao.

Amesema kuwa licha ya bunge kupitisha mswada wa mabadiliko ya sheria za uchaguzi siku chache kabla ya marudio ya uchaguzi , aliheshimu maoni ya wengine ikiwemo sababu kuwa angebadilisha sheria za mchezo unaoendelea ndio maana hakutia sahihi.

Kadhalka ameahidi kumtumikia kila mkenya bila ubaguzi wowote ikizingatiwa kuwa uchaguzi ni kipindi tu cha kuteua viongozi ila huduma ni kwa kila mwananchi kwa mujibu wa katiba.

Haya yanajiri huku muungano wa NASA ukipinga uchaguzi huo na kusisitiza kuwa ni sharti kufanyike uchaguzi mwengine katika kipindi cha siku 90.

Total Views: 213 ,