Rais Uhuru atetea pendekezo la mabadiliko ya sheria za uchaguzi

Rais Uhuru Kenyatta ametetea pendekezo la chama cha Jubilee la kufanyia marekebisho sheria ya uchaguzi akisema hatua hiyo itaondoa mianya iliyosababisha kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais na mahakama ya juu.

Rais Kenyatta alisema mabadiliko hayo yatahakikisha uchaguzi utafanywa kwa uwazi kwani yatapunguza dosari za kiuchaguzi.

Akiongea mjini Busia leo rais Kenyatta aliyeandamana na naibu wake William Ruto aliwashukuru wakazi wa kaunti hiyo kwa kumpigia kura kwa wingi wakati wa uchaguzi wa agosti na akawahimiza kujitokeza kwa wingi wakati wa marudio.

Aidha naibu wa rais William Ruto alisema upinzani hauko tayari kushiriki kwenye uchaguzi huo kwa vile umebaini utashindwa akisisitiza kuwa chama cha Jubilee kiko tayari kwa uchaguzi jinsi ilivyoagizwa na mahakama ya juu.

Mwisho

Total Views: 216 ,