Rais awaonya wafisadi

Rais Uhuru Kenyatta ametoa onyo kali kwa maafisa wa utumishi wa umma wanaotumia vibaya rasilimali za umma akisema mtu yeyote atakayepatikana akifuja fedha za umma atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akikiri kwamba baadhi ya watu wamejihusisha kwenye ufisadi na kujinufaisha na rasilimali za umma, rais Kenyatta ameonya kwamba watumishi wa umma sharti wawe na uadilifu na siku ambapo watu hawakuwajibikia vitendo vyao zimepita.

Akiongea leo katika majengo ya bunge alipotoa hotuba ya kuangazia hali ya taifa, rais alihimiza idara ya mahakama kutekeleza jukumu lake kuhakikisha kwamba watu hawapokei maagizo ya kiholela kutoka kwa mahakama ili kukwepa utekelezaji haki.

Kadhalika rais amewahimiza wabunge kuratibu sheria muafaka ambazo zitasaidia kwenye vita dhidi ya ufisadi.

Hata hivyo rais alisema uzinduzi wa mfumo wa digitali kwenye utoaji huduma za serikali umesaidia kuziba mianya iliyotumiwa kutekeleza ufisadi.

Kadhalika alifichua kwamba mwaka uliopita pekee, nchi hii iliweza kutwaa mali ya umma ya thamani ya shilingi milioni tano ambayo ilikuwa imeibwa.

Amehimiza kuwepo juhudi za pamoja za Wakenya wote wakiwemo wale wa sekta ya kibinafsi ili kuhakikisha maadili ya kikatiba yanazingatiwa.

Mwisho

Total Views: 225 ,