Mtengo aibuka Mshindi Malindi

Willy Baraka Mtengo wa chama cha ODM ndiye mbunge mpya mteule wa Malindi kaunti ya Kilifi baada ya kumpiku Philip Charo wa chama cha Jubilee kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi mdogo ulioandaliwa jana Jumatatu katika eneo hilo.

Mtengo alipata jumla ya kura elfu kumi na tano mia tano themanini na mbili dhidi ya kura elfu tisa mia mbili arobaini na tatu za Philip Charo huku Attas Shariff aliyekamata nafasi ya tatu akijizolea jumla ya kura elfu moja mia tano na arobaini na saba.

Uchaguzi huo mdogo ulivutia jumla ya wagombezi saba lakini ukageuka na kuwa kinayang’anyiro baina ya Jubilee na Cord huku muungano wa upinzani ukishinda kiti hicho.

Matokeo ya uchaguzi huo huenda yamedhihirisha jinsi mrengo wa upinzani ulivyodhibiti siasa za eneo la Pwani.

Wakati huo huo tume ya uchaguzi IEBC imemtangaza Aaron Cheruiyot wa Jubilee kama mshindi wa uchaguzi mdogo wa useneta katika kaunti ya Kericho baada ya kujizolea jumla ya kura elfu mia moja na tisa,mia tatu hamsini na nane dhidi ya kura elfu hamsini na sita,mia tatu na saba za Paul Sang wa chama cha Kanu

Total Views: 424 ,