Maafisa wa KWS wapigwa Kalamu kufuatia vifo vya vifaru

Maafisa sita wakuu wa shirika la huduma kwa wanyama pori wamesimamishwa kazi huku uchunguzi ukianzishwa kuhusiana na kifo cha kutatanisha cha kifaru wa kumi katika mbuga ya kitaifa ya wanyama pori ya Tsavo mashariki.

Kulingana na ripoti ya uchunguzi huru iliyotolewa na waziri wa utalii Najib Balala,huenda utepetevu wa maafisa wa shirika hilo wakati wa kuwahamisha vifaru hao ulisababisha vifo hivyo.

Akitoa ripoti hiyo waziri wa utalii Najib Balala amesema kuwa vifaru hao walifariki kutokana na athari iliyotokana na kunywa maji yaliyokuwa na nyumvi zaidi ya yale waliyokuwa wakinywa kutoka kwa mbuga waliyohamishwa.

Amedokeza kuwa kutokana na uchunguzi wa upasuaji na pia wa maabara ,ilibainika kuwa wanyama hao walikaukiwa na viwango vya maji mwilini swala linalodaiwa kutokana na kutojali kwa maafisa husika.

Jumla ya vifaru kumi na wanne walipangiwa kuhamishwa ila shughuli hiyo ikasitishwa kufuatia vifo hivyo huku takwimu kutoka kwa shirika la World Wildlife Fund zikionyesha kuwa ni vifaru 5,400 pekee walio hai.

Mwisho

Total Views: 175 ,