Diamond Kufanyika Uswizi

Mashindano ya “Diamond League”yanayoandaliwa na shirikisho la riadha duniani IAAF , yataandaliwa jijini Zurich, Uswizi Alhamisi hii kisha yakamilike jijini Brussels, Ubelgiji tarehe moja mwezi ujao.

Washindi kumi na wanane wa dunia watawania ubingwa katika mashindano hayo ambapo watagawana dola milioni moja nukta sita za Marekani. Jijini Zurich, Moh Farah, mmoja wa wanariadha weledi atashiriki kwa mara ya mwisho katika mbio za viwanjani kabla hajaanza kushiriki kwenye mbio za barabarani na zile za masafa marefu. Wanaume watakinzana katika mbio za mita 100, 400, 1500, 5000, na mbio za mita mia nne kupokezana kijiti.

Mkenya Elijah Managoi aliyetwaa nishani ya dhahabu katika mashindano ya riadha duniani yaliyoandaliwa jijini London, atajitosa ugani mashindano haya yatakapong’oa nanga.

Wanawake watashindana katika fani za mbio za mita 200, mita 800, mita elfu tatu kuruka vihunzi na kidimbwi cha maji.

Total Views: 227 ,