Cha Mtema Kuni kwa Wauguzi Wanaogoma

Huduma ya taifa ya polisi leo imetoa onyo kwa wauguzi wanaogoma kufuatia agizo la rais la Uhuru Kenyatta kuwataka kurejea kazini kufikia kesho ijumaa.

Kwenye taarifa inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinnet ameufahamisha umma kwamba makamanda wote husika wameagizwa kuhakikisha kwamba wauguzi ambao wanataka kurudi kazini wafanye hivyo bila kutatizwa.

Ameongeza kuwa usalama utazidi kuimarishwa katika hospitali za umma na yeyote atakayepatikana akifanya vitendo kinyume cha sheria atachukuliwa hatua kali.

Haya yanajiri siku moja baada ya rais Uhuru Kenyatta kuwaagiza wauguzi wote katika hospitali za umma wanaoshiriki mgomo kufuata agizo la mahakama ya leba na kurejea kazini kesho saa mbili asubuhi kinyume na hilo wafutwe kazi.

Hata hivyo wahudumu hao wa afya jana kupitia katibu wa muungano wao Seth Panyako waliapa kuendelea na mgomo wakisema unalindwa kisheria.

Total Views: 94 ,